Historia Fupi ya Maisha ya
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran
Ayatullah Udhmaa Sayyid Ali Khamenei (daama dhilluh)
"Mtafuteni mtu mmoja mfano wa Sayyid Khamenei ambaye
ameshikamana barabara na Uislamu na ni mtumishi wa umma,
na ambaye amedhamiria kwa dhati ya moyo kulitumikia taifa hili,
muone kama mtampata mtu kama huyo aliye mfano wake yeye.
Mimi ninamjua yeye kwa miaka mingi."
Imam Khomeini (quddisa sirruh)
Tangu Kuzaliwa Kwake hadi Kuanza Masomo
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran Ayatullah Udhmaa Sayyid Ali Khamenei ni mwana wa marehemu Hujjatul Islam wal Muslimin al-Haj Sayyid Jawad Husaini Khamenei. Alizaliwa katika mji mtakatifu wa Mashhad, tarehe 28 Safar (Mfunguo Tano) mwaka 1358 Hijria, mwafaka na tarehe 18 Aprili 1939 Miladia. Yeye ni mwana wa pili wa kiume katika tumbo lao. Maisha ya baba yake yaani Sayyid Jawad Khamenei yalikuwa ya kawaida kabisa kama yalivyo ya wengi wa masheikh, wanazuoni, na waalimu wa masomo ya dini. Mkewe na wanawe walijifunza mengi mazuri kutoka kwake yeye mwenyewe mzee huyo, hasa juu ya maana halisi ya kukinai na kutosheka pamoja na kuishi maisha yasiyo na makuu, kiasi kwamba sifa mbili hizo zikawa ni miongoni mwa matendo yaliyopamba maisha yao ya kila siku.Katika Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza)
Baada ya kumaliza masomo ya sekondari ambako pia alisoma vitabu vya lugha na
sarufi ya Kiarabu, k.v. Jami'u 'l-Muqaddamaat, Sayyid Ali Khamenei alijiunga na
Hawza (chuo kikuu cha kidini) ambako alianza kujifunza kwa baba yake na walimu
wengine fasihi na masomo mengine ya kimsingi. Kuhusu kujiunga kwake na chuo cha
kidini anasema: "Baba yangu ndiye aliyekuwa sababu kuu ya mimi kuichagua njia
hii ya nuru ya kusomea taaluma za dini; na mama yangu naye pia alipendelea jambo
hilo na kunishajiisha pia".
Alisoma katika madrasa za Sulayman Khan na Nawwab, huku baba yake akiwa
anasimamia na kufuatilia masomo yake. Katika awamu hiyo alisoma pia kitabu cha
Ma'aalim. Kisha baada ya hapo akasoma kwa baba yake na pia kwa kiwango fulani
kwa marehemu Sheikh Mirza Mudarris Yazdi vitabu vya kifikihi vya vya Sharai'u
'l-Islam na Sharh al-Lummah. Aidha alisoma vitabu vingine vya kifikihi na
kiusuli, k.v. Rasa'il na Makasib kwa marehemu Sheikh Hashim Qazwini; na masomo
yaliyobakia ya usul na fikihi katika kiwango cha kati (sat'h) alisomeshwa na
baba yake. Ni jambo la kushangaza na lililo nadra sana kuona kwamba alifanikiwa
kukamilisha masomo yote ya shahada ya msingi (muqaddamaat) na ya kati (sat'h)
katika muda wa miaka mitano na nusu tu. Katika muda wake wote huo wa masomo,
baba yake, marehemu Sayyid Jawad alikuwa na nafasi muhimu katika maendeleo ya
mwanawe huyo hodari. Katika upande wa mantiki na falsafa, Sayyid Ali Khamenei
alisoma kitabu cha taaluma hizo cha Mandhumah cha Sabzwari, kwanza kwa marehemu
Ayatullah Mirza Jawad Agha Tehrani na baadaye kwa marehemu Sheikh Ridha Eisi.
Katika Hawza ya Najaf al-Ashraf
Akiwa na umri wa miaka 18, Ayatullah Khamenei alianza kuhudhuria darsa za khariji (masomo ya juu kabisa) katika taaluma ya fikihi na usuli kwa marjaa mkubwa wa wakati huo - Ayatullah Udhmaa Milani. Mnamo mwaka 1957, alifunga safari ya kuelekea mjini Najaf al-Ashraf kwa ajili kuzuru maeneo matakatifu. Baada ya kujionea mwenyewe na kushiriki pia katika darsa za khariji za mujtahidi wakubwa wa Hawza ya Najaf akiwemo marehemu Sayyid Muhsin Hakim, Sayyid Mahmud Shahrudi, Mirza Baqir Zanjani, Sayyid Yahya Yazdi na Mirza Hasan Bojnurdi, Sayyid Ali Khamenei alivutiwa na kupendezwa na hali ya masomo hapo, mfumo wa usomeshaji na uhakiki wake, hivyo akamjulisha baba yake nia yake ya kuendelea na masomo huko, lakini baba yake hakukubaliana na wazo hilo. Hivyo, baada ya muda akarejea Mashhad.Katika Hawza ya Qum
Kuanzia mwaka 1958 hadi 1964 Ayatullah Khamenei aliendelea na masomo ya juu kabisa ya fikihi, usuli na falsafa katika Hawza ya Qum na kufaidika na elimu za maulamaa wakubwa wakubwa, k.v. marehemu Ayatullah Udhmaa Borujerdi, Imam Khomeini, Sheikh Murtadha Haeri Yazdi na Allama Tabatabai. Mnamo mwaka 1964, walipokuwa wakiandikiana barua, Ayatullah Khamenei aligundua kwamba jicho moja la mzazi wake lilikuwa na mtoto, hivyo alihuzunika mno. Akiwa katika hali ya njia panda baina ya kubaki Qum na kuendelea na masomo katika chuo muhimu cha kidini cha mji huo na kurudi Mash-had kwa ajili ya kwenda kumtunza na kumhudumia baba yake, mwishowe Ayatullah Khamenei alifikia uamuzi wa kurudi Mashhad kwa ajili ya kumtunza na kumshughulikia baba yake. Akizungumzia kuhusu uamuzi wake huo, Ayatullah Khamenei anasema: "Nilielekea Mashhad; na Mwenyezi Mungu Mtukufu alinipa taufiki kubwa. Alakullihali nilikwenda huko kutekeleza wajibu wangu. Kama kuna taufiki nimepata katika maisha yangu, naamini kwamba imetokana na wema huo nilioufanya kwa baba yangu au niseme kwa wazazi wangu." Kwa hakika, katika kuchagua moja kati ya njia mbili hizo, Ayatullah Khamenei alichagua njia sahihi zaidi. Baadhi ya walimu na watu aliokuwa akijuana nao walikuwa wakisikitika kwa nini aliamua kuondoka Qum mapema kiasi hicho, na kwamba laiti angebaki hapo, angekuja kuwa hivi na vile kimafanikio katika mustakabali. Hata hivyo, baadaye ilibainika kuwa uamuzi aliochukua ulikuwa sahihi, na kwamba takdiri ya Mwenyezi Mungu ilikuwa imemwekea majaaliwa mengine na yaliyo bora zaidi ya yale waliyokuwa wakifikiria wao. Je, kuna mtu aliyeweza hata kuwaza na kufikiria kwamba katika enzi hizo aalimu huyo kijana mwenye kipawa akiwa na umri wa miaka 25, aliyeamua kwa sababu ya kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu kuondoka Qum na kurudi Mashhad ili kwenda kuwatunza na kuwashugulikia wazazi wake, miaka 25 baadaye angekuja fikia daraja ya juu ya kuwa kiongozi wa Umma wa Kiislamu? Aliporudi Mashhad hadi mwaka 1969, Ayatullah Khamenei aliendelea kusoma fikihi na usuli kwa maulamaa wakubwa wa Hawza ya Mashhad na hasa kwa Ayatullah Milani; na hakusitisha masomo yake isipokuwa katika siku za mapumziko au zile alizokuwa akijishughulisha na mapambano au alipokuwa safarini na kifungoni. Aidha kuanzia mwaka 1964 ambapo aliamua kubaki rasmi huko Mashhad kwa ajili ya kusoma na kumtunza baba yake ambaye alikuw amekwishakuwa mzee na mgonjwa, Ayatullah Khamenei alijishughulisha pia na kuwasomesha wanafunzi wa masomo ya kidini na wale wa vyuo vikuu vitabu vya kifikihi, kiusuli na mafunzo mengine ya dini.Harakati za Kisiasa
Bega kwa Bega na Harakati za Imam Khomeini (quddisa sirruh)
Tokea mwaka 1962, wakati Ayatullah Khamenei alipokuwa katika mji wa Qum na pale zilipoanza harakati za kimapinduzi na za upinzani za Imam Khomeini dhidi ya siasa za kupiga vita Uislamu na kuikumbatia Marekani za Muhammad Reza Pahlavi, aliingia kwenye uwanja wa mapambano ya kisiasa, ambapo licha ya taabu, mashaka, mateso, kutupwa gerezani na kupelekwa uhamishoni, kwa muda wa miaka 16 kamili aliendelea na mapambano katika njia hiyo bila ya kuhofu hatari yoyote. Kwa mara ya kwanza katika Muharram ya mwaka 1959, Ayatullah Khamenei alipewa jukumu na Imam Khomeini la kwenda kufikisha ujumbe kwa Ayatullah Milani pamoja na maulamaa wengine wa Khorasan, juu ya namna ya kupanga mikakati ya kampeni zitakazoendeshwa na maulamaa wakati wa mwezi wa Muharram za kufichua kwa wananchi siasa za Shah za kujikumbatisha kwa Marekani na juu ya hali ya nchi pamoja na matukio yaliyojiri Qum. Alitekeleza kazi hiyo aliyopewa, kisha yeye mwenyewe akaelekea mji wa Birjand kwa ajili ya tablighi na kufikisha ujumbe wa Imam Khomeini wa kufichua maovu ya utawala wa Kipahlavi na Marekani. Kwa sababu hiyo, tarehe 9 Muharram sawa na tarehe pili Juni mwaka 1963, Ayatullah Khamenei alitiwa nguvuni na kuwekwa rumande hadi siku ya pili yake ambapo aliachiwa huru kwa sharti kwamba asije akapanda mimbari na kutoa hotuba, na pia awe akifatiliwa nyendo zake. Kufuatia kujiri kwa tukio la Khordad 15 (Juni 5) Ayatullah Khamenei aliondolewa Birjand na kupelekwa Mash-had, akakabidhiwa kwenye mahabusu ya kijeshi na kuwekwa rumande kwa muda wa siku kumi huku akikabiliana na mazingira magumu kabisa ya maudhi na mateso.Kutiwa Nguvuni Mara ya Pili
Katika mwezi wa Januari mwaka 1964 (Ramadhan 1383), Ayatullah Khamenei pamoja na wenzake kadhaa walipanga mkakati maalumu wa safari ya kuelekea Kerman. Baada ya kusimama kwa siku mbili tatu huko Kerman na kuhutubia na kukutana na maulamaa na wanafunzi wa kidini wa mji huo, waliendelea na safari yao hadi Zahedan. Hotuba kali na za hamasa za Ayatullah Khamenei ziliwavutia wananchi, na hasa zile alizotoa katika siku za kumbukumbu ya tarehe 26 Januari, siku ambayo ulifanyika uchaguzi bandia wa kura za maoni uliopangwa na Shah. Tarehe 15 Ramadhani ambayo ilisadifiana na siku ya kuzaliwa Imam Hasan AS, ushujaa, hamasa ya kimapinduzi na ujasiri ulioonyeshwa na Ayatullah Khamenei wa kufichua siasa za kishetani za Marekani na utawala wa Kipahlavi, zilifikia kilele chake kiasi kwamba usiku huohuo alitiwa nguvuni na Savak (askari wa usalama) na kusafirishwa kwa ndege hadi Tehran. Kwa muda wa karibu miezi miwili, Ayatullah Khamenei aliwekwa katika seli ya peke yake kwenye jela ya Qezel Qal'eh na kukabiliana na kila aina ya mateso na manyanyaso.Kutiwa Nguvuni Mara ya Tatu na ya Nne
Darsa zake za tafsiri ya Qur'ani, hadithi na fikra za Kiislamu katika miji ya Mashhad na Tehran zilihudhuriwa kwa wingi mno na vijana wengi waliokuwa na hamasa kubwa ya kimapinduzi. Harakati zake hizo ziliwaghadhibisha Savak na hivyo wakaanza kumfuatilia. Kutokana na hali hiyo, katika mwaka 1967 Ayatullah Khamenei akawa anaishi kwa kujificha katika mji wa Tehran, na mwaka mmoja baadaye, yaani mwaka 1968, alitiwa nguvuni na kuwekwa korokoroni. Harakati hizo za kielimu na uwekaji vikao, usomeshaji na utoaji hotuba za kuiamsha na kuirekebisha jamii, ndizo zilizopelekea mnamo mwaka 1971 akamatwa tena na kikosi cha usalama (Savak) cha utawala wa Shah na kutiwa jela.Kutiwa Nguvuni Mara ya Tano
Akizungumzia kutiwa nguvuni kwake kwa mara ya tano na Savak, Ayatullah Khamenei (Allah ampe umri) amesema: "Kuanzia mwaka 1970, mazingira ya kuanzishwa harakati za mtutu wa bunduki yalianza kuhisika nchini Iran. Harakati za vyombo vya utawala wa wakati huo za kunifuatilia mimi zilikuwa kubwa mno na zikazidi kuongezeka kwa sababu vilihisi kwamba haingewezekana kuwepo harakati kama hizo bila kuwa na mahusiano na watu kama mimi. Mwaka wa 1971 na kwa mara ya tano nilitiwa jela tena. Vitendo vya kikatili vilivyokuwa vikifanywa na Savak huko jela, vilionyesha dhahiri kuwa vyombo vya dola vilikuwa na hofu kubwa ya kuungana harakati za mapambano ya silaha na zile za fikra za Kiislamu, na havikuwa tayari kukubali kwamba harakati zangu za kifikra na kitablighi za Mashhad na Tehran hazikuwa na mfungamano na harakati hizo. Baada ya kuachiwa huru, wigo wa darsa zangu za tafsiri kwa watu wote na zile za siri za masuala ya kiitikadi zilizidi kuongezeka."
Kutiwa Nguvuni Mara ya Sita
Kati ya mwaka 1971-1974 darsa za tafsiri ya Qur'ani na masuala ya kiidiliojia (kiitikadi) za Ayatullah Khamenei zilikuwa zikifanyika katika misikiti mitatu: Karamat, Imam Hasan AS na Mirza Jaafar huko Mashhad na kuvutia watu wengi hasa vijana waelewa, walioamka kifikra, na wanafunzi wanamapinduzi wa kidini ambao walipata fursa ya kuelewa fikra sahihi za Kiislamu. Darsa zake za Nahju 'l-Balagha, nazo pia zilikuwa na msisimko na hali ya aina yake, na zikawa zinachapishwa na kukathiriwa na mashine ya kurudufia kwa jina la "Nuru kutoka kwenye Nahju 'l-Balagha" na kusambazwa mkono mwa mkono. Wanafunzi vijana wanamapinduzi wa kidini ambao walikuwa wakisoma kwa Ayatullah Khamenei darsa juu ya ukweli na mapambano, walikuwa wakielekea kwenye miji ya mbali na karibu ya Iran kuziamsha fikra za wananchi kwa kuwaelimisha juu ya masuala hayo na kutayarisha mazingira kwa ajili ya mapinduzi makubwa ya Kiislamu.Uhamishoni
Mwishoni mwa mwaka 1977, utawala wa kinyama wa Kipahlavi ulimtia nguvuni Ayatullah Khamenei na kumpeleka uhamishoni kwa muda wa miaka mitatu huko kwenye mji wa Iranshahr. Katikati ya mwaka 1978 wakati harakati za mapambano ya wananchi Waislamu na wanamapinduzi wa Iran zilipokuwa zimepamba moto, Ayatullah Khamenei aliachiwa huru huko uhamishoni na hivyo kurejea mjini Mashhad ambako alijiunga kwenye safu ya mbele ya mapambano ya wananchi dhidi ya utawala katili wa Kipahlavi. Mwishowe, baada ya miaka 15 ya mapambano ya kishujaa, jihadi na subra katika njia ya Mwenyezi Mungu, na kuvumilia kila aina ya taabu, shida na machungu, aliyashuhudia matunda ya mapambano hayo, ambayo yalikuwa ni ushindi wa mapinduzi makubwa ya Kiislamu ya Iran na kuanguka kiidhilali kwa utawala wa kidhalimu wa Kipahlavi na kusimamishwa utawala wa Kiislamu katika ardhi ya Iran.Karibu na Ushindi wa Mapinduzi
Uandishi na Utafiti
1. Nadharia Jumla ya Fikra za Kiislamu katika ya Quran